Francis Godwin, Iringa
Ajali ya Iringa |
JINAMIZI la ajali limeutikisa mkoa baada
ya watu 12 kufa na wengine 31 kujeruhiwa kwenye ajali mbili tofauti ndani ya
saa sita za usiku mmoja.
Hali hiyo ambayo imeacha simanzi kubwa
kwa wananchi wa hapa na mikoa jirani ya Njombe na Mbeya, usiku wa kuamkia jana ililiza
wananchi wa Tanangozi, Kalenga kutokana na wananchi wake tisa kufa papo hapo huku
18 wakijeruhiwa.
Hiyo ilitokana na ajali iliyotokea saa
11.45 jioni juzi baada ya lori namba T 970 AJT lililokuwa likiendeshwa na
Francis Peter kutoka Mbeya kuja mjini hapa kugonga gari dogo aina ya Toyota Hiace
namba T 920 DBA lililokuwa likiendeshwa na Sebastian Njau.
Wananchi wa hapa hususan wa Ulete ambako
Hiace ilikuwa ikienmda wakiwa na wakati mgumu wa kutaka kujua majina ya ndugu waliopoteza
maisha kwenye ajali hiyo hadi saa 4 usiku walikuwa eneo la ajali Tanangozi.
Hapo walikuwa na viongozi mbali mbali wa
Polisi na Serikali chini ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza ambapo pia
saa 5 usiku ajali nyingine ikatokea kwa basi la Ngasamo Express lililokuwa likitoka
Mwanza kwenda Mbeya lilipopinduka Mafinga.
Mashuhuda wa tukio hilo waliozungumza na
mwandishi wa habari hizi wakiwa eneo la tukio Tanangozi, walidai kuwa Hiace ni
mali ya Kastoli Maluli na ilisimama kushusha abiria na wakati ikiondoka ndipo lori
hilo lililofeli breki likaipamia.
John Kalinga alisema kutokana na lori
kuwa kwenye mwendo kasi, nusu ya abiria waliokuwa kulia walipoteza maisha huku
baadhi ya miili ikinyofoka mikono na miguu na kukutwa kwenye lori umbali wa zaidi
ya meta 15 kutoka ilipokuwa Hiace.
Hata hivyo, shuhuda huyo alisema miili mingi
ni ya wanaume na kwamba madereva wa magari yote walinusurika na kukimbizwa kwenye
hospitali ya Rufaa ya Mkoa.
Inasemekana baadhi ya majeruhi na waliopoteza
maisha kwenye ajali hiyo walikuwa ni waenda kwa miguu.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Julius Mjengi
alithibitisha kutokea kwa ajali hizo.
Alisema basi lililopinduka lilikuwa
likiendeshwa na Amos Yoyo na kuwa majeruhi wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya
ya Mufindi mjini Mafinga na miili ya marehemu imehifadhiwa kwenye mochari ya
hospitali hiyo.
Kutokana na ajali hizo, Masenza aliiagiza
Polisi kuanzisha ukaguzi wa magari yote na kuchukua hatua kali.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Julius
Mjengi (wa pili kulia) akitazama mabaki ya Toyota iliyogongwa na lori eneo la
Tanangozi, Iringa, juzi usiku. (picha na Francis Godwin).
0 comments:
Post a Comment