Wafanyabiashara Kariakoo wahofia kufilisika

Mwandishi Wetu

WAFANYABIASHARA wadogo wa Soko la Kariakoo Dar es Salaam wanahofia kufilisika hivyo kumwomba Rais John Magufuli aingilie kati tozo mpya za Shirika la Viwango Tanzania (TBS). 

Wakizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, wafanyabiashara hao walidai kuwa kwa takribani wiki moja sasa wameshindwa kutoa hata kontena moja bandarini kwa sababu ya gharama kubwa wanazotozwa.

TBS imeanzisha utaratibu mpya wa kulipisha faini mizigo inayoingia nchini ambayo haikukaguliwa wakati iko nchini China faini ambayo ni asilimia 15 ya thamani ya mzigo ulioingia.

Wafanyabiashara wa Kariakoo wenye mitaji midogo huagiza mizigo kutoka nje kwa kushirikiana na   kuagiza kwa pamoja kwa kutumia kontena moja.

Lakini kwa mujibu wa taratibu za TBS katika ukaguzi nje ya nchi, mizigo midogo yenye thamani ya chini ya dola 10,000 za Marekani huwa haikaguliwi lakini inapofika nchini na kuonekana haijakaguliwa, wafanyabiashara hao hupigwa faini.

Mohammed Mmasi alisema wafanyabiashara wengi wa Kariakoo hununua mizigo kidogo kidogo na kuunganisha kupata shehena moja kubwa, ili kupata nafuu ya gharama za kusafirisha.

Na pia kwamba hatua hiyo imewezesha vijana wengi wenye mitaji midogo kushiriki biashara na kukuza mitaji yao.

Mmasi alisema kwa sasa kuna hatari ya vijana na wanawake kukosa uwezo wa kuendelea kufanya biashara kutokana na kutozwa tozo ya TBS asilimia 15 ya thamani ya mzigo (CIF), kiwango ambacho ni chini kidogo ya VAT.

“Kwa hiyo kijana mwenye mzigo wa nguo zenye thamani ya dola 10,000 talipa ushuru wa forodha asilimia 25, VAT asilimia 18, ushuru wa bidhaa asilimia 10 na TBS asilimia 15.

“Hii maana yake ni kwamba atalipa asilimia 68 ya thamani ya mzigo wake kama kodi ambayo ni sawa na dola 6,800. Sasa kijana huyu atauza mzigo wake kwa shilingi ngapi?” Alihoji Mmasi.

Sandaland Yenga, alisema wanamwomba Rais Magufuli aingilie kati suala hilo, kwani kama mfumo huo utaendelea, wafanyabiashara wadogo watafilisika.

“Utaratibu wa zamani wa wafanyabiashara wadogo kushirikiana uliwezesha vijana wengi wenye mitaji midogo kushiriki biashara na kukuza mitaji yao.

“Kwa sasa, biashara kubwa inayofanyika Kariakoo ni  ya Watanzania kuagiza bidhaa kutoka China na kuziweka kwenye maduka yao na vifungashio vyao na   watu kutoka nchi jirani kuzinunua na kuzipeleka kwao. Nchi huingiza fedha za kigeni kwa njia hiyo,” alisema.

Tanzania hivi sasa inafanya ukaguzi wa bidhaa zote zinazoingia nchini ili kudhibiti ubora. Ukaguzi huu unafanyika bidhaa zinakonunuliwa kabla ya kuletwa nchini.

Mwanzoni, bidhaa kama magari tu ndizo zilikaguliwa lakini baadaye serikali ikaona ni bora kukagua zote.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo