JPM: Rudisheni posho za Mwenge


*Ni waliotaka kwenda Simiyu kuuzima
*Siku ambayo anakumbukwa Nyerere

Fidelis Butahe na Suleiman Msuya

UAMUZI wa Rais John Magufuli kuagiza viongozi wote wa Serikali walioalikwa sherehe za Kilele cha Mbio za Mwenge kutohudhuria hafla hiyo ili kubana matumizi, kimepongezwa na watu wa kada mbalimbali nchini, huku wakihoji sababu za jambo hilo kutofanyika tangu miaka ya nyuma.

Wamesema uamuzi huo unaonesha kwamba kiongozi mkuu huyo wa nchi ana lengo la kuinua uchumi wa Taifa.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro akionesha wasiwasi kwamba huenda kufutwa kwa sherehe kunatokana na Serikali kukabiliwa na ukata, aliitaka kuliweka wazi jambo hilo.

Jana Rais aliagiza viongozi hao walioalikwa kuhudhuria sherehe hizo zinazofanyika kitaifa kesho wilayani Bariadi mkoani Simiyu, kutohudhuria na kutaka waliokwishalipwa fedha za posho na safari kwa ajili hiyo wazirejeshe.

Taarifa iliyotolewa jana Ikulu Dar es Salaam na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi ilieleza kuwa Rais alitoa maagizo hayo ikiwa ni utekelezaji wa azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kubana matumizi yasiyo ya lazima na kuelekeza rasilimali nyingi katika shughuli za maendeleo ya nchi.

Viongozi waliotajwa kutakiwa kufuta safari zao za Bariadi ni pamoja na wakuu wote wa mikoa, wilaya, wakurugenzi wa mamlaka ya serikali za mitaa, mameya na wenyeviti wa halmashauri za majiji, manispaa, miji na wilaya pamoja na watumishi ambao hufuatana nao wakiwamo madereva na wasaidizi wao ambao kwa idadi hufikia takribani 1,500.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Kitivo cha Sheria, Dk Onesmo Kyauke alisema uamuzi huo ni sahihi na kuhoji sababu za kufanyika sasa, wakati Mwenge umekuwa ukizunguka muda mrefu.

Dk Kyauke alisema fedha hizo zinapaswa zielekezwe katika miradi ya kijamii kwani inakabiliwa na changamoto nyingi zinazowazunguka.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Lusekelo Kasongwa alisema uamuzi wa Rais na Serikali ni mzuri na kutakiwa kuungwa mkono.

Kasongwa alisema hakuna sababu ya jamii kufikiri uamuzi huo unahusu hali ya uchumi nchini, kwani Serikali ina mambo mengi ya kufanya kuliko sherehe.

“Uamuzi huo wa Rais ni wa kuungwa mkono, ila jambo la msingi ni kuhakikisha kuwa uamuzi huo uoneshe faida yake kwenye jamii,” alisema.

Dk Jamal Sadick, ambaye ni mtaalamu wa mifupa alisema jitihada hizo zimejikita kuinua uchumi wa nchi hivyo ni vema jamii ikamwunga mkono na si kulalamika.

“Wapo watu waliozoea mteremko; safari za mara kwa mara, hivyo kwa sasa hali imekuwa kinyume najua inawauma, lakini tumpe nafasi abadilishe mfumo na tutafaidi wote, sidhani kuwa sherehe hizo zina faida ya moja kwa moja kwa jamii,” alisema.

Kwa kuwa sherehe za kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru huambatana na maadhimisho ya siku ya kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere aliyefariki dunia miaka 17 iliyopita, agizo hilo linawataka viongozi wote wa mikoa na wilaya, kubaki katika maeneo yao ya kazi na kujiwekea utaratibu wa jinsi ya kuenzi siku hiyo.

Aidha, Rais aliagiza wilaya zote zilizofanya vizuri kwenye shughuli za maendeleo wakati Mwenge ukiwa katika maeneo yao, zitambuliwe kwa kutangazwa rasmi katika kilele cha Mbio za Mwenge na zawadi zilizoandaliwa zitapelekwa kwa wahusika kwa taratibu utakaoelekezwa na Mamlaka husika kutoa zawadi hizo.

Katika maelezo yake, Rais alisema kutokana na umuhimu wa Mwenge viongozi wote wa Simiyu wajitokeze kwa wingi kushiriki sherehe za kuzima Mwenge, ambako mgeni rasmi atakuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein.


Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo